Wananchi wa mkoa wa Iringa na mikoa jirani wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupima ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi

Posted on: January 20th, 2021

Wananchi wa mkoa wa Iringa na mikoa jirani wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupima ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi ambao kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa wanasema wanawake laki tatu hufariki kila mwaka kutokana na ugonjwa huo.

Saratani ya shingo ya kizazi,ni ugonjwa ambao huathiri wanawake kuanzia umri wa miaka 23 na kuendelea na husababishwa na kirusi kiitwacho Human Papilloma, virusi hivi binadamu anapata kwa njia ya kujamiiana.

Mganga mkuu kutoka hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa Dr Alfred Mwakalebela amesema ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi unaua watu wengi hasa katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.

Mwakalebela ametaja sababu zinazosababisha saratani ya shingo ya kizazi ni pamoja na mapenzi katika umri mdogo, kuwa na wapenzi wengi, uzazi mkubwa yaani kuzaa watoto kuanzia watoto watano na kuendelea, na ndoa za wake wengi pia ni sababu.

 Vile vile amesema katika nchi zinzazoendelea watu wengi wanashindwa kufikia huduma za afya,na hali ya umasikini inayofanya watoto wadogo kujiingiza katika biashara ya ngono ili kukidhi mahitaji yao ya kila siku.

Amesema ili kupunguza tatizo la saratani nchini ni vyema wananchi wa Mkoa wa Iringa wakafika katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa ili kufanyiwa uchunguzi kwani wengi wa wagonjwa hugundulika wakiwa katika hali mbaya.

Dr. ametoa wito kwa wananchi kuendelea kujitokeza kufanyiwa uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi na kupatiwa matibabu  yake mapema, ambapo uchunguzi na matibabu ya awali ni bure kabisa.

Pia Waziri wa afya,maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto Dr. Dorothy Gwajima ametoa rai kwa wananchi kuwa na tabia ya kupima afya mara kwa mara kwani 75% ya wagonjwa hufika hospitali wakiwa na hali mbaya.

Wizara ya afya nchini Tanzania imesema kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wapya wa saratani nchini wapatao 51, 000 na inakadiriwa ifikapo mwaka 2030 kutakuwa na ongezeko la wagonjwa wapya.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa wanawake [300,000] laki tatu hufariki kila mwaka kutokana na saratani ya shingo ya kizazi na mwezi january hutumuka kutoa uelewa kwa jamii juu ya ugonjwa huu.

Na Zainabu Mlimbila

Iringa RRH